TAARIFA YA MKURUGENZI WA TUME YA KIKRISTU YA HUDUMA ZA
JAMII (CSSC) KWA MHE. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DK. JAKAYA MRISHO
KIKWETE KATIKA UZINDUZI WA JENGO LA MAABARA YA HOSPITAL YA WILAYA YA UKEREWE-TAREHE
7-SEPTEMBA-2013
MHE RAIS:
Tume ya kikristu ya Huduma
za Jamii (CSSC) kupitia mradi wake
wa ART inaratibu huduma za kupunguza maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto
na pia huduma za tiba kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (yaani WAVIU)
katika wilaya zote za mkoa wa Mwanza ikiwemo wilaya ya Ukerewe. Mradi huu
unafadhiliwa na watu wa Marekani kupitia
taasisi yake ya CDC. Mpaka sasa mradi huu wa ART unaratibu huduma katika
vituo vya tiba vipatavyo 69 (9 Ukerewe)
na vituo vya kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto vipatavyo 311 (29 Ukerewe) mkoani Mwanza. CSSC kwa kushirikiana na kamati ya usimamizi
wa afya ya mkoa, kamati za usimamizi wa afya za wilaya na wadau wengine,
imekuwa inachangia utoaji wa huduma hizi katika maeneo yafuatayo:- Ushauri wa
kitaalamu (Technical Assistance), mafunzo kwa watumishi, madawa na vifaa tiba
pamoja na rasilimali fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli endelevu za tiba
ya Ukimwi.
Mbele yako ni jengo la kisasa la maabara utakalolizindua
leo lililojengwa kwa ufadhili wa watu wa Marekani kupitia taasisi yake ya
Centers for Disease Control and Prevention (CDC) katika mkakati wake wa
kuchangia upatikanaji wa huduma bora na salama za maabara nchini. Maabara hii
ni mojawapo ya maabara sita za wilaya nchini zilizofaidika na mkakati huu, nyingine
ni Bagamoyo (Pwani), Ludewa (Njombe, Siha (Kilimanjaro), Karume (Kilimanjaro)
na Micheweni (Pemba).
Hadi kukamilika kwa ujenzi huu, wadau mbali mbali
walishiriki kwa namna moja ama nyingine katika kuufanikisha ujenzi huu wakiwemo
kamati ya Usimamizi wa afya ya mkoa wa Mwanza, kamati ya usimamizi wa afya ya
wilaya ya Ukerewe na washirika wenzetu wa AIDSRelief/LEAD
waliokuwa wadau wa Ukimwi hapo awali na pamoja na timu ya maabara ya CDC Tanzania.
Matarajio ya CSSC
ni kuona maboresho haya ya miundombinu ya maabara hii yanachangia kwa kiasi
kikubwa katika ufuatiliaji wa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi waliojiunga
na huduma za tiba wilayani Ukerewe (routine clinical assessment) pamoja na
kutoa huduma bora za kiuchunguzi kwa wagonjwa katika hospitali hii ya wilaya.
Vile vile kurahisisha kwa kiasi kikubwa ufuatiliaji wakaribu wa watoto na wakina mama wajawazito wenye maambukizi
katika kipindi hiki ambapo mikoa sita ya Tanzania ukiwemo mkoa wa Mwanza
inaanza kutekeleza mkakati wa utoaji wa huduma za kuzuia maambukizi toka kwa
mama kwenda kwa mtoto wa Option B plus. Ambapo mama mjamzito
mwenye maambukizi ataanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi-ARV mara moja pindi anapogundulika kuwa
na maambukizi, ili kupunguza kiwango cha maambukizi toka asilimia 26 (2011) kwenda asilimia
5 ifikapo mwaka 2015 na kufikia malengo ya kuwa na kizazi salama kisicho na
maambukizi nchini.
MHE RAIS:
Mwisho ninaomba kukupongeza wewe binafsi pamoja na serikali
za Tanzania na Marekani kwa kazi kubwa iliyofanyika katika kuboresha huduma endelevu za tiba hapa nchini. CSSC itaendelea kushirikiana kwa karibu
na serikali katika ngazi ya taifa, mkoa na wilaya pamoja na wadau wote wa afya
mkoani Mwanza katika kuboresha afya za wanaoishi na virusi vya ukimwi ili
waweze kushiriki katika shughuli za maendeleo.
MHE RAIS: NAOMBA KUWASILISHA!
No comments:
Post a Comment